Kenya imeimarisha juhudi za kuongeza idadi ya watalii wanaozuru taifa hili, amesema Rais William Ruto.
Huku lengo likiwa ni kufikisha watali milioni tano wanaozuru nchi hii kufikia mwaka 2027, Rais William Ruto alisema kampeni hiyo inalenga kuitangaza Kenya kuwa nyumbani kwa kivutio muhimu ambacho ni bora kwa uvumbuzi, michezo, mikutano, wanyamapori na likizo.
“Tunapanua bidhaa za utalii zaidi ya wanyamapori, Mbuga za Kitaifa na fuo za baharini. Uvumbuzi za kidijitali, michezo makongamano na utamaduni ni miongoni mwa vivutio tulivyo navyo,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa aliyasema hayo leo Alhamisi, alipofungua rasmi maonyesho ya kuhama kwa Kongoni kwa ushirikiano na kampuni ya utangazaji ya China barani Afrika, katika mbuga ya kitaifa ya Masai Mara, kaunti ya Narok.
Zoezi hilo la kuhama kwa Kongoni huwavutia watalii wengi wa hapa nchini na wale wa kimataifa, huku hoteli zikijaa pomoni kwa lengo la kushuhudia tukio hilo la kustajabisha.
Kongoni hao huvuka mto Mara, katika vituo tofauti, huku mamba wakiwasubiri kwa hamu isiyo kifani. Vita vya majini kati ya kongoni hao na mamba hupamba zoezi hilo, ambapo kila mtalii hujizatiti asipitwe na tukio hilo.