Serikali kushirikiana na sekta ya kibinafsi kwa ukuzaji wa lishe ya mifugo

Tom Mathinji
1 Min Read

Wizara ya kilimo imesema serikali itakodisha ardhi ya serikali isiyotumika kwa wawekezaji wa kibinafsi, ili kukuza mahindi ya manjano kwa ajili ya uzalishaji wa chakula cha mifugo.

Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, alisema mpango huo utaongeza uzalishaji wa mahindi ya manjano na kupunguza utegemezi wa nchi katika uagizaji wa mahindi ya manjano yanayotumika katika uzalishaji wa chakula cha mifugo.

Akizungumza katika kiwanda cha Maziwa cha Wakulima kilichopo Mukurwe-ini, Nyeri, Kagwe alisema, ushirikiano huo na sekta ya kibinafsi utapunguza gharama ya vyakula vya mifugo na gharama ya juu ya pembejeo za kilimo katika sekta ya kilimo.

Kauli yake inajiri miezi mitatu baada ya Wizara yake kuidhinisha uingizaji wa zaidi ya magunia milioni 5.5 ya mahindi ya manjano yasiyo ya GMO, ili yatumike kwa uzalishaji wa chakula cha mifugo.

TAGGED:
Share This Article