Zaidi ya Wazee na Vijana 200 waliokuwa na ghadhabu, wametembea kwa miguu umbali za kilomita 80, kulalamikia kuibwa kwa mifugo wao katika eneo la ADC Mutara, Rumuruti, Laikipia Magharibi.
Kulingana na wakazi hao, visa vya wizi wa mifugo vimeongezeka ambapo zaidi ya ng’ombe 200 wameibiwa ndani ya mwezi mmoja pekee.
Katika tukio la hivi karibuni, ng’ombe saba waliibwa, hatua iliyochochea wakazi hao kuandamana hadi katika kituo cha polisi cha Wiyumiririe wakiwashinikiza maafisa wa polisi kuwasaidia kuwapata mifugo hao.
Aidha wakazi hao waliwashutumu maafisa wa polisi kwa kushirikiana na wahalifu katika eneo hilo, hasaa baada ya washukiwa wawili wa wizi wa mifugo kuachiliwa huru kutoka korokoro za polisi.
“Tuliwakamata washukiwa watatu, lakini tukashangaa wawili kati yao waliachiliwa bila maelezo ya kuridhisha,” alisema Joseph Sigoei, mmoja wa wakazi.
“Ndiyo maana tulitembea zaidi ya kilomita 70 hadi kwao ili kutafuta ng’ombe wetu. Tunaamini polisi wa Rumuruti na Wiyumiririe wanashirikiana na wezi wa mifugo, na tunataka uchunguzi wa kina,” aliongeza Singoei.
Wakazi hao walivamia nyumba ya mshukiwa mmoja na kuwapata ng’ombe waliokuwa wameibiwa kabla ya polisi kuingilia kati na kuwapeleka wanyama hao katika kituo cha polisi.
Kipsang Kisorio, mkazi mwingine, alielezea hali kuwa mbaya zaidi. “Watoto wetu sasa wanakunywa chai bila maziwa,” alilalamika. “Ng’ombe hawa ndiyo maisha yetu. Kuibiwa kwao si pigo la kiuchumi tu, ni jambo la moyoni.”
Kamanda wa Polisi wa Laikipia Magharibi, Francis Ng’ang’a, alithibitisha kuwa uchunguzi unaendelea na akawaomba wakazi kujiepusha kujichukulia sheria mikononi mwao.
“Tunaelewa hasira zao, lakini ni muhimu sheria ifuate mkondo wake,” alisema Ng’ang;a.
Boniface Morogo, mkazi wa Rumuruti, amemwomba Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kuingilia kati haraka na kutoa suluhisho la kudumu kwa mzozo huo.
“Tumepiga kelele kwa muda mrefu lakini hakuna anayetusikiliza. Tunahitaji serikali kuu kuingilia kati mara moja,” alisema Morogo.