Wanariadha 58 wameteuliwa kuiwakilisha Kenya katika Makala ya 20 ya mashindano ya Riadha Duniani mjini Tokyo, Japan, kati ya Septemba 13 na 21 mwaka huu.
Kikosi hicho kimeteuliwa baada ya kukamilika kwa majaribio ya kitaifa yaliyoandaliwa katika uwanja wa Ulinzi Complex kaunti ya Nairobi siku ya Jumanne.
Baadhi ya wanariadha waliojumuisha kikosini ni mabingwa watetezi Faith Kipyegon atakayeshiriki mbio za mita 1500 na mita 5,000, Mary Moraa atakayetetea taji ya mita 800, mabingwa wa Olimpiki Emmanuel Wanyonyi mita 800 na Beatrice Chebet mita 5,000 na 10, 000.
Wanariadha wengine watakaoshiriki mashindano hayo ya dunia kwa mara ya kwanza wakiwemo Clinton Aluvi, Edmund Serem, Margaret Akidor, Ishmael Rokitto, Dorcas Ewoi, Sarah Moraa, Lillian Odira, Mercy Oketch, George Mutinda, Brian Tinega, Doris Lemngole, Pamela Kosgei, Janeth Chepngetich na Edwin Kurgat.
Kenya inapania kuboresha matokeo ya mwaka 2023 mjini Budapest, Hungary, ilikozoa dhahabu tatu, fedha tatu na shaba 4.