Ufugaji samaki: Wimbi jipya la matumaini kwa jamii ya wafugaji Marsabit

Martin Mwanje
5 Min Read

Ufugaji wa samaki ambao hapo awali haukufikirika kabisa miongoni mwa jamii za wafugaji, sasa unakuwa tegemeo jipya kwa mamia ya wakazi wa kaunti ya Marsabit. Hii ni kutokana na juhudi za uhamasishaji na mafunzo ya kujengea jamii uwezo, yanayoendeshwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa ushirikiano na Serikali ya kaunti ya Marsabit, kufuatia ukame mkubwa uliolikumba eneo hilo kati ya mwaka 2019 hadi 2022.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mpango wa Maendeleo ya Mazingira Chalbi, Mzee Katelo Guyo, mradi huu hauhusu tu samaki, bali pia ni njia ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kujenga jamii yenye uwezo wa kustahimili misukosuko ya hali ya hewa.

Alipoanzisha kikundi chake mwaka 2023, kilikuwa na wanachama 15 pekee. Leo hii, kina wanachama 40 na idadi inaendelea kuongezeka kwa kasi. Wanawake kama Hadija Guyo sasa wamo mstari wa mbele.

Kwa Hadija, samaki si chakula tu—ni matumaini mapya baada ya miaka mingi ya kutegemea msaada wa chakula.

Aidha, ufugaji wa samaki umekuwa njia ya kujikomboa kiuchumi na kuleta usawa wa kijinsia. Anasema kuwa kikundi chao hutumia mapato kutoka kwa mauzo ya samaki kwa ajili ya kuweka akiba, kukopeshana, na kukuza biashara kupitia vikundi vya akiba na mikopo (table banking).

Katika Taasisi ya Mafunzo ya Ufundi ya North Horr, ufugaji wa samaki sasa ni sehemu ya mtaala. Masomo hayo yanaunganisha kilimo, lishe, na elimu ya biashara.

Kwa Abudho Galgallo, mwanafunzi wa kilimo katika taasisi hiyo, bwawa la samaki si mradi wa darasani tu—ni mfano hai wa mabadiliko yanayowezekana kwa jamii nzima.

Adho Game, mwanafunzi wa stashahada ya kilimo katika taasisi hiyo, alisimulia jinsi ambavyo hakuwa amewahi kula samaki hapo awali, lakini sasa ni shabiki mkubwa na huwashauri wengine waonje. Anaamini kuwa ufugaji wa samaki unaweza kuwa suluhisho la ajira kwa vijana iwapo wataukumbatia.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa taasisi hiyo, Sammy Malingu, alisema kuwa mabwawa ya samaki katika taasisi hiyo yanawapa wanafunzi ujuzi wa vitendo kupitia mbinu ya kujifunza kwa kufanya.

Kwa upande wake, Kephas Juma, Mkuu wa Idara ya Kilimo katika taasisi hiyo, alisema kuwa wanafunzi wanakuwa mabalozi wa ufugaji wa samaki katika vijiji vyao.

Wataalamu wa lishe pia wanaona fursa kubwa ya kukabiliana na utapiamlo kupitia ulaji wa protini zitokanazo na samaki, hasa katika maeneo yaliyo hatarini kama North Horr.

Anastacia Mutiti, Mkuu wa Idara ya Lishe katika taasisi hiyo, alisema kuwa samaki wana protini nyingi na asidi muhimu za amino ambazo zinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha utapiamlo iwapo jamii itaukubali kwa wingi.

Katika Moyale, eneo lingine linalokumbwa na njaa, Musa Hassan Dida amegeuza ufugaji wa samaki kuwa hadithi ya mafanikio.

“Nilianza na vijisamaki 300. Baada ya miezi sita, niliwauza kwa shilingi elfu sabini na tano. Sasa nina 500, na wateja hunitafuta kila siku,” alisema Musa, akitambua mchango wa WFP na serikali ya kaunti katika kumpatia msaada wa kitaalamu na vifaa.

Kupitia mapato ya samaki, Musa sasa anahudumia familia yake nzima, ikiwemo kugharimia matibabu ya baba yake ambaye anasumbuliwa na shinikizo la damu jijini Nairobi.

Idara ya Uvuvi ya Serikali ya Kaunti ya Marsabit kwa kushirikiana na mashirika kama WFP, ndiyo injini ya mabadiliko haya. Wanatoa vifaa kama mipira ya kufunika mabwawa, vifaranga vya samaki, chakula cha samaki na ushauri wa kitaalamu kwa wakulima wapya wa samaki katika kaunti hii kame ya wafugaji.

Sostine Wanjala, Afisa wa Uvuvi wa Kaunti ya Marsabit, alisema kuwa imani potovu na tamaduni za zamani zilichangia mitazamo hasi kuhusu ulaji wa samaki miongoni mwa jamii za wafugaji.

Hata hivyo, kupitia kampeni za “Kula Samaki” zinazofanyika kote kaunti hiyo, idadi ya wafugaji wa samaki imeongezeka kutoka watu 15 mwaka 2023 hadi zaidi ya watu 100 mwaka huu.

Albert Mwambulu, Afisa wa Ugavi kutoka Shirika la WFP, alisema kuwa lengo lao ni kugeuza ufugaji wa samaki kuwa nyenzo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuhakikisha usalama wa chakula na kuboresha lishe. Na katika Marsabit, ndoto hiyo inatimia.

Wakulima wapya wa samaki wamepongeza juhudi za serikali ya kaunti pamoja na WFP kwa kuwawezesha kuanzisha na kukuza shughuli zao mpya, hali ambayo imepunguza kwa kiwango kikubwa utegemezi wao kwa msaada wa chakula, hasa wakati wa ukame unaojirudia mara kwa mara.

Share This Article