Simanzi imetanda katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kakamega kufuatia kifo cha mwanafunzi wa kidato cha tatu, David Owino Oduor, kilichotokea jana Jumapili jioni wakati akicheza mpira na wenzake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Julius Mambili, mwanafunzi huyo alianguka ghafla akiwa uwanjani na alikimbizwa katika Hospitali Kuu ya Kakamega, ambako alithibitishwa kufariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali hapo.
Ingawa chanzo rasmi cha kifo bado hakijabainika, inaripotiwa kuwa huenda marehemu alikuwa na tatizo la moyo.
Uchunguzi wa kitabibu unatarajiwa kufanyika ili kubaini kilichosababisha kifo hicho.
Kamanda wa Polisi wa eneo la Kakamega ya Kati, Vincent Cherutich, amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya kaunti ya Kakamega huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
Marehemu Owino alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliotajwa kuwa na nidhamu nzuri na pia alitegemewa siyo tu uwanja na bali pia darasani.
Kifo chake kimesemakana kuacha pengo kubwa katika shule hiyo.