Viongozi wanawake nchini wamemwomboleza marehemu Dkt. Phoebe Asiyo wakimtaja kuwa mtetezi mashuhuri wa haki za wanawake na usawa wa kijinsia.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake nchini (MYWO) Rahab Mwikali, viongozi hao aidha wamesema Dkt. Asiyo alitekeleza wajibu mkubwa katika kuwachochea wanawake kujiunga na ulingo wa siasa.
“Sauto yake ilileta mabadiliko makubwa nchini,” alisema Mwikali wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatatu.
Dkt. Asiyo atakumbukwa kama afisa mkuu mwandamizi wa kwanza mwanamke wa Idara ya Magereza nchini Kenya.
Aidha, alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza waliochaguliwa kuliwakilisha eneo bunge la Karachuonyo.
Isitoshe, alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa MYWO baada ya kuchaguliwa kuhudumu kwenye wadhifa huo mnamo mwaka wa 1958.
Dkt. Asiyo alifariki Julai 17 wakati akipokea matibabu nchini Marekani.
Alikuwa na umri wa miaka 93.