Mshukiwa mkuu wa mauaji ya hivi punde katika Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta, KNH Kennedy Kalombotole amefikishwa mahakamani leo Jumatatu.
Kennedy Kalombotole alifikishwa katika mahakama ya Kibera akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mgonjwa Edward Maingi Ndegwa.
Ndegwa alipatikana ameuawa katika wadi nambari saba ya hospitali hiyo Julai 11 mwaka huu.

Mahakama imempa Kiongozi wa Mashtaka (DPP) siku tatu kuwasilisha ripoti za matibabu juu ya mshukiwa kabla ya kutoa uamuzi kuhusiana na ombi la kumzuia kwa siku 21.
Uamuzi juu ya ombi hilo utatolewa Julai 24.
Ripoti zinaashiria mshukiwa huyo alikuwa alilazwa katika hospitali ya KNH Disemba 1 mwaka 2024.
Aidha, anashukiwa kuhusika katika mauaji mengine ya mgonjwa Gilbert Kinyua Muthoni aliyekuwa na umri wa miaka 40.
Mauaji ya Kinyua yalitokea baina ya usiku wa Februari 6 na 7 mwaka huu.
Katika mauaji ya hivi punde, polisi walibaini kuwa mshukiwa aliingia katika wadi ya ghorofa ya saba alikokuwa amelazwa Maingi usiku wa manane na kumdunga kisu.
Hospitali ya Kenyatta inasema mshukiwa alikuwa mgonjwa wa muda mrefu wa hospitali hiyo na kwamba ililazimika kumpa mahali pa kujisitiri kwani hana makazi.