Pombe haramu imenaswa huko Kisumu kufuatia msako mkali uliofanywa na maafisa kutoka kituo cha polisi cha Kisumu Central.
Maafisa wa polisi kutoka kituo hicho walifanya msako huo Julai 20 baada ya kudokezewa na raia ilipo pombe hiyo.
Wakati wa msako huo, maafisa walipata pombe ikiwa imehifadhiwa kwenye mitungi 10 ya lita 20 kila moja, mapipa mawili ya lita 200 kila moja ikiwa na pombe aina ya Kangara na lita 5 za pombe aina ya chang’aa.
Pombe hiyo ilikuwa imefichwa kichakani.
https://x.com/NPSOfficial_KE/status/1947011871393067189/video/1
Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS, inasema uchunguzi wa awali unaashiria kuwa kichaka hicho kilikuwa kikitumika kama ghala ya muda ya Kangara kabla ya kusafirishwa kwa ajili ya utoneshaji wake.
“Mshukiwa mmoja, anayeaminika kuwa mmiliki wa pombe hiyo, alikamatwa katika eneo hilo na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho (leo Jumatatu,” ilisema NPS kwenye taarifa.
NPS imewapongeza raia kwa ushirikiano wao katika kukabiliana na jinamizi la pombe haramu katika eneo hilo.