Chama cha wakulima cha Pesi chachukua hatua kudhibiti matumizi ya kemikali haramu

Dismas Otuke
6 Min Read

Chama cha Ushirika wa Wakulima cha Pesi kilichoko katika kaunti ndogo ya Aberdare, kaunti ya Nyandarua, kimechukua hatua madhubuti kudhibiti matumizi ya dawa za kilimo miongoni mwa wanachama wake.

Hii ni kufuatia madai kuwa viazi vinavyolimwa katika eneo hilo vina mabaki ya kemikali ambazo hazijakubalika kwa matumizi ya kilimo.

Hatua hii imejiri baada ya ripoti ya Chuo Kikuu cha Egerton kudai kuwa baadhi ya viazi kutoka Nyandarua vina mabaki ya viuatilifu hatari.

Kwa kujibu, chama hicho chenye wanachama zaidi ya 1,400 kimeanza kuuza kemikali zilizoidhinishwa pekee katika maduka yake rasmi, ambapo wakulima wanatakiwa kununua pembejeo zao kupitia chama ili kuhakikisha usalama na uwajibikaji.

Akizungumza na wanahabari, mwenyekiti wa chama hicho Francis Ngana alisema hatua hiyo ni ya tahadhari, hata kama ripoti yenyewe inapingwa na baadhi ya viongozi.

“Tunachukulia madai hayo kama hadithi, lakini tumeamua kuchukua hatua halisi. Hatutaruhusu wakulima wetu kununua dawa kiholela. Tukipoteza imani ya walaji, sekta nzima ya viazi itaporomoka,” alisema.

Ripoti ya Egerton ilionya kwamba matumizi ya viuatilifu visivyoidhinishwa vinaweza kusababisha athari za kiafya kwa walaji, yakiwemo matatizo ya homoni, sumu mwilini, na kupotea kwa virutubisho vya viazi.

Ingawa taarifa hizo zimezua wasiwasi, Gavana wa Nyandarua Kiarie Badilisha,amepinga vikali ripoti hiyo akisema haina msingi wa kisayansi.

“Hatujapokea ripoti rasmi au iliyopitiwa kitaaluma inayothibitisha madai hayo. Wakulima wetu wanazingatia sheria. Nyandarua bado ni kitovu cha mazao salama na bora,” alisema.

Licha ya matamshi ya Gavana, Ngana alisema ni muhimu kuchukua tahadhari kwa sababu athari za soko ni kubwa ikiwa walaji watapoteza imani kwa mazao ya eneo hilo.

Mbali na suala la kemikali, chama hicho pia kinakumbwa na matatizo ya miundombinu na huduma za kimsingi.

Mwezi mmoja uliopita, transfoma ya Kenya Power iliibwa katika kituo cha biashara cha Pesi na kusababisha kukatizwa kwa huduma muhimu ya baridi kwa maziwa.

Kwa sasa, chama hicho kinatumia takriban shilingi 10,000 kila siku kusafirisha maziwa hadi mji wa Shamata, umbali wa zaidi ya kilomita 30, ambapo kuna jokofu linalofanya kazi.

Ngana alisema kuwa wizi huo pia ulichelewesha uzinduzi wa gala jipya la kuhifadhi viazi, ambalo lilikuwa limejengwa kusaidia wakulima kutunza mazao yao hadi bei sokoni iwe nzuri.

Kukosekana kwa ghala hiyo kumewaacha wakulima katika hatari ya hasara na unyonyaji wa madalali.

Hali hii inazidishwa na ubovu wa barabara ya kilomita tano inayounganisha kituo cha Pesi na barabara kuu ya Nyahururu–Nyeri.

Barabara hiyo huwa haipitiki wakati wa mvua, na kusababisha kuchelewa kwa usafirishaji wa maziwa na mazao ya mashambani.

Mkulima wa eneo hilo, Bi. Susan Kimaru kutoka eneo bunge la Ndaragwa, alisema kuwa hali mbaya ya barabara imechangia kushuka kwa bei za mazao na kuwavunja moyo wakulima.

“Gunia la viazi linauzwa kwa kati ya shilingi 800 hadi 1,000. Hii haitoshi kulipa hata gharama zetu. Wakati barabara ni mbaya, madalali hujaa hapa na kununua kwa bei ya kutupa,” alisema.

Bi. Kimaru aliongeza kuwa eneo lao hutegemea sana Kaunti jirani ya Nyeri kwa masoko ya mboga, jambo linaloongeza gharama za usafirishaji na kuwaweka wakulima katika hali ya kutegemea walanguzi.

Wakati huo huo, Mbunge wa Ol Kalou, Mheshimiwa David Kiaraho, amelaumu vikali shirika la Kenya Power kwa kushindwa kulinda miundombinu ya umeme.

Alisema kuwa visa vya wizi wa transfoma vimeongezeka katika maeneo ya Ol Kalou, Ndaragwa na hata pembezoni mwa mji wa Nyahururu, Kaunti ya Laikipia.

Kulingana na mbunge huyo, wezi hao wanaonekana kuwa watu walio na ujuzi wa kitaalamu na huenda wakawa wafanyakazi wa zamani au watu wanaoshirikiana na wafanyakazi wa kampuni hiyo.

“Transfoma zinang’olewa kwa ustadi mkubwa. Hawa si wezi wa kawaida. Tunaangazia kwa karibu wakandarasi walioko ndani ya kampuni ya Kenya Power,” alisema Kiaraho. Alionya kuwa uchunguzi unaendelea na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika. “Nataka kuwaambia wanaohusika kwamba siku zao zimehesabiwa. Wizi wa transfoma huathiri shule, zahanati, biashara na wakulima. Hatuwezi kukubali maendeleo yetu kubatilishwa na wahalifu wachache.”

Wakulima wa eneo la Pesi sasa wanatoa wito kwa serikali kuu na serikali ya kaunti kuingilia kati haraka ili kurejesha huduma za umeme, kutengeneza barabara na kulinda sifa ya kilimo cha Nyandarua. Kwa mujibu wa Bw. Ngana, jamii hiyo tayari imechukua hatua za kuhakikisha matumizi salama ya pembejeo, na sasa wanahitaji msaada wa serikali ili kuimarisha miundombinu na usalama wa shughuli zao.

“Tumechukua hatua. Tunahitaji msaada wa miundombinu, usalama na masoko. Tusipotendewa haki, juhudi zetu zitakuwa bure,” aliongeza.

Kadri mjadala kuhusu matumizi ya kemikali mashambani unavyoendelea, wadau wa sekta ya kilimo wanakubaliana kuwa hatua za haraka na za pamoja zinahitajika ili kulinda usalama wa chakula na kipato cha wakulima katika eneo hili muhimu la uzalishaji nchini Kenya.

Share This Article