KNH: Mshukiwa wa mauaji alikuwa mgonjwa wetu wa muda mrefu

Martin Mwanje
2 Min Read
Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.

Mshukiwa wa mauaji ya wagonjwa wawili katika Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta, KNH alikuwa mgonjwa wa muda mrefu katika hospitali hiyo. 

KNH pia inasema Kennedy Kalombotole pia hakuwa na makazi.

Kennedy Kalombotole – Mshukiwa wa mauaji katika hospitali ya KNH

Mshukiwa huyo alilazwa KNH Disemba 1 mwaka 2024, na pia alishukiwa kuhusika katika mauaji mengine ya mgonjwa Gilbert Kinyua aliyekuwa na umri wa miaka 40, baina ya usiku wa Februari 6 na 7 mwaka huu.

Hospitali hiyo imeyasema hiyo baada ya kuibuka kwa taarifa jana Alhamisi kuwa mgonjwa mwingine kwa jina Edward Maingi, alipatikana akiwa amefariki hospitalini hapo.

Maingi alilazwa hospitalini hapo Julai 11, 2025.

Akizungumzia kisa hicho leo Ijumaa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. William Sigilai alisema Kalombotole tayari alikuwa akichunguzwa kuhusiana na mauaji ya awali ya Kinyua.

Dkt. Sigilai alisema mgonjwa aliyeuwa hivi punde alipatikana akiwa amefariki muda mfupi baada ya saa nane mchana, wakati muda wa kuwatembelea wagonjwa ulipokamilika.

“Mnamo Julai 17, 2025 saa nane mchana, punde tu baada ya muda wa kuwaona wagonjwa kukamilika,  mgonjwa alipatikana kwenye wodi ya wagonjwa akiwa ameloa damu. Mgonjwa huyo alifanyiwa uchunguzi na kubainishwa kuwa amefariki,” alisema Dkt. Sigilai.

Polisi wa ujasusi kutoka kitengo cha mauaji tayari wamemkamata Kalombotole kuhusiana na mauaji hayo.

Katika mauaji hayo ya hivi punde, polisi walibaini kuwa mshukiwa aliingia katika wodi ya ghorofa ya saba alikokuwa amelazwa Maingi usiku wa manane na kumdunga kisu.

Kalombotole kwa sasa yuko korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashataka ya mauaji.

TAGGED:
Share This Article