Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen leo Ijumaa ametoa maelekezo yake ya kwanza ya sera juu ya maafisa wa polisi kutumia mabavu na silaha.
Akiwahutubia wanahabari baada ya kumtembelea Gavana wa Samburu Lati Lelelit ofisini mwake mjini Maralal, Murkomen alitangaza utoaji wa sera hiyo inayolenga kutoa mwongozo juu ya matumizi ya mabavu na silaha kwa maafisa wa polisi kote nchini.
“Nimetoa maelekezo ya sera juu ya matumizi ya mabavu na silaha kwa mujibu wa Kifungu 245(4) cha Katiba, Sheria ya Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS) na maamuzi ya mahakama kwa Inspekta Mkuu wa Polisi (IG),” alisema Murkomen.
“Nimemtumia IG sera hiyo ikielezea mapendekezo ya kina juu ya matumizi ya mabavu kwa kuzingatia mpangokazi uliopo wa sheria na maamuzi ya mahakama.”
Akizungumza wakati wa kuanza kwa mikutano ya Jukwaa la Usalama mjini Samburu iliyolenga kujadili hofu ya usalama na utoaji huduma kwa wakazi, Waziri huyo alisema hii ni sera yake ya kwanza tangu aliposhika hatamu za uongozi wa wizara hiyo.
“Hii itatoa mwongozo wa matumizi ya mabavu na silaha mahali popote katika kujilinda na kulinda umma na kuhakikisha usalama wa taifa.“
IG anatakiwa kuwaelezea maafisa wake yaliyomo kwenye sera hiyo.
Sera hiyo inakuja wakati ambapo maafisa wa polisi wanakabiliwa na wimbl la shutuma kutokana na madai kuwa wana hulka ya kuwafyatulia risasi raia bila sababu za msingi, hata kama hawajajihami kwa silaha.
Kiasi kwamba maafisa kadhaa wa polisi wameshtakiwa kuhusiana na madai ya kuwafyatulia risasi raia, akiwemo mmoja anayetuhumiwa kumpiga risasi mchuuzi wa barakoa jijini Nairobi.
Mchuuzi huyo baadaye alifariki wakati akitibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta, KNH.