Wakenya wazoa dhahabu tatu Nigeria, mashindano ya Chipukizi Afrika

Nahodha wa Kenya Clinton Aluvi Wamatinya alinyakua dhahabu ya mita 100 kitengo cha chini ya umri wa miaka 20 kwa muda wa sekunde 10.42.

Dismas Otuke
2 Min Read

Wanariadha wa Kenya walizoa dhahabu tatu katika siku ya pili ya Makala ya Tatu ya Mashindano ya Riadha barani Afrika kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 18 na walio chini ya miaka 20 uwanjani Moshood Abiola mjini Abeokuta, Nigeria.

Nahodha wa Kenya Clinton Aluvi Wamatinya alinyakua dhahabu ya mita 100 kitengo cha chini ya umri wa miaka 20 kwa muda wa sekunde 10.42.

Nishani ya fedha ilitwaliwa na Letebele Karabo kutoka Afrika Kusini huku John Caleb wa Nigeria akiridhia shaba.

Cynthia Chepkirui alishinda dhahabu ya pili katika mita 3000 chini ya umri wa miaka 18 kwa muda wa dakika 9 sekunde 26.35.

Emmanuel Lemiso na Brian Kiptoo walinyakua dhahabu na fedha katika mita 2000 kuruka viunzi na maji chini ya umri wa miaka 18.

Wakenya pia walishinda medali za fedha katika mita 1500 kwa wanaume na wanawake chini ya umri wa miaka 18.

Owan Logorodi alishinda nishani ya fedha ya wanaume huku Sheila Chepng’etich akitwaa fedha ya wanawake.

Chepng’etich pia alishinda fedha nyingine katika mita 3000 chini ya umri wa miaka 20 kwa kutumia dakika 8 sekunde 43.98, nyuma ya Mganda Bentalin Yeko aliyeibuka mshindi kwa dakika 8 sekunde 45.99, huku shaba ikimwendea Asmaa Bassou wa Morocco.

Mashindano hayo yanaendelea leo na yatakamilika kesho Jumamosi.

Share This Article