Mbunge wa zamani wa Karachuonyo Dkt. Phoebe Muga Asiyo amefariki.
Dkt. Asiyo alifariki katika jimbo la North Carolina nchini Marekani wakati akipokea matibabu.
“Tafadhali tunaomba uelewa na uvumilivu wako wakati tukikabiliana na wakati huu mgumu. Maelezo ya kina juu ya ibada za kumbukumbu na matayarisho ya mazishi yatatolewa hivi karibuni,” alisema Caesar Asiyo kwenye taarifa ya kutangaza kifo cha mbunge huyo wa zamani.
“Waliomfahamu wataukosa mno uwepo na upendo wake.”
Marehemu Asiyo atakumbukwa kuwa mwanawake wa kwanza kuchaguliwa bungeni katika eneo la Nyanza na kujitosa katika ulingo wa kisiasa nchini.
Hii ilikuwa katika ya 1970 na 1990 wakati ambapo kulikuwa na ukame wa vongozi wanawake nchini.
Aidha, Dkt. Asiyo alitekeleza wajibu muhimu katika kuwanoa makali na kuwatia moyo viongozi wengine wanawake, kama vile aliyekuwa mbunge wa Kitui Central Charity Ngilu, kujitosa katika ulingo wa kisiasa.
Dkt. Asiyo pia aliwahi kulifanyia kazi Shirika la Umoja wa Mataifa, UN na Shirika la Maendeleo ya Wanawake.
Alikuwa pia mtetezi shupavu wa haki za binadamu akipigania hasa masuala yanaohusu watoto na wanawake.