Mwimbaji wa Kenya Bensoul ni mmoja wa wanamuziki tajika ambao wamewasili nchini Uganda kwa ajili ya sherehe ya kusikiliza mkusanyiko wa nyimbo uliopatiwa jina la “Cartel Bizness” za mwanamuziki wa Uganda Denim Cartel.
Sherehe hiyo itaandaliwa Jumapili Julai 20, 2025 ndani ya klabu ya usiku iitwayo Silo 15, iliyoko Bugolobi jijini Kampala nchini Uganda.
Denim Kartel ambaye anaingilia kazi ya utayarishaji muziki atakuwa anaonjesha watakaohudhuria sherehe hiyo nyimbo hizo ambazo ni za mitindo mbali mbali na ambazo huenda zikatikisa Afrika Mashariki.
Kazi hizo zitatolewa kwa umma Julai 23, 2025.
Denim Kartel ambaye humotishwa na wanamuziki kama Dr. Dre, Wizkid, Pharrell Williams, Kanye West na Timbaland anasema hatayarishi tu muziki bali pia anabadili mdundo wa bara hili la Afrika.
Wanamuziki ambao wamethibitishwa kuhudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Elijah Kitaka, Kamanzi, Mike Kayihura, A Pass, Bensoul, Big Tril, Tungi na DJ Vanz.
Denim Cartel alishirikiana na Axon ambaye ni mmoja wa watayarishaji bora wa muziki nchini Uganda katika maandalizi ya kazi hiyo.