Connie Francis afariki akiwa na umri wa miaka 87

Connie amekuwa hospitali tangu mwanzo wa mwezi huu wa Julai lakini ugonjwa aliokuwa akiugua haukufichuliwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji na mwigizaji wa Marekani Connie Francis, amefariki akiwa na umri wa miaka 87. Haya ni kulingana na rafiki yake wa muda mrefu Ron Roberts aliyechapisha habari hizo kwenye Facebook.

Haya yanajiri wiki mbili tu baada ya mwimbaji huyo wa wimbo uliotamba sana hivi karibuni “Pretty Little Baby” kuripotiwa kulazwa hospitalini katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Wimbo huo ambao umetumiwa na watu wengi kwenye mitandao ya kijamii katika muda wa wiki chache zilizopita, ulitolewa mwaka 1962.

Katika ujumbe wake Ron alisema kwamba Connie angekuwepo, angekubaliana naye kwamba mashabiki zake ndio wa kwanza kufahamu kuhusu kifo chake. Aliahidi kwamba taarifa zaidi zitatolewa baadaye.

Connie aliinuka na kuwa mmoja wa waimbaji bora wa miaka ya 1950 hadi 1960, ambapo nyimbo zake zimeorodheshwa kati ya nyimbo kumi bora mara kadhaa.

Yeye ndiye alikuwa mwanamuziki wa kwanza wa kike kuwahi kuwa namba moja kwenye orodha ya Billboard Hot 100 kutokana na wimbo wake uitwao “Everybody’s Somebody’s Fool”.

Taaluma yake ilikumbwa pia na masaibu pale ambapo alikaribia kuachwa na kampuni iliyokuwa ikimsimamia ya MGM Records mwaka 1957.

Babake alimshauri akarekodi wimbo uitwao “Who’s Sorry Now?” kama njia ya kujinusuru asiachiliwe na kampuni hiyo na kwa bahati nzuri wimbo huo ulimuinua hata zaidi.

Baya jingine lililowahi kumkuta mwimbaji huyo ni wakati alibakwa kwenye chumba cha hoteli huko Long Island mwaka 1974. Lililofuatia ni kupoteza sauti yake miaka mitatu baadaye kufuatia upasuaji aliofanyiwa.

Connie amekuwa hospitali tangu mwanzo wa mwezi huu wa Julai lakini ugonjwa aliokuwa akiugua haukufichuliwa. Rafiki yake Ron alitangaza kwamba alikwenda hospitali kufanyiwa vipimo kufahamu kilichokuwa kikimsababishia maumivu makali.

Ameacha mtoto mmoja wa kiume aitwaye Joseph Garzilli Jr.

Share This Article