DRC na Rwanda: Baraza la Mawaziri la Rwanda laidhinisha makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani

Martin Mwanje
1 Min Read
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio (kulia) aliungana na viongozi wenzake Thérèse Kayikwamba wa DR Congo na Olivier Nduhungirehe wa Rwanda kutia saini tamko la maelewano yaliyowezesha makubaliano ya amani kati ya nchi hizo mbili

Baraza la Mawaziri la Rwanda limeidhinisha makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani baina yake na DRC na kuahidi kujitolea kuyaunga mkono.

Tovuti inayounga mkono serikali ya The New Times imeripoti kuwa makubaliano hayo “yanawakilisha hatua muhimu katika kushughulikia maswala ya usalama wa Rwanda, kurejesha amani na utulivu katika Kanda ya Maziwa Makuu, na kukuza ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda”.

Ilinukuu taarifa kutoka kwa Baraza la Mawaziri kufuatia mkutano wa kikao hicho ulioongozwa na Rais Paul Kagame jana Jumatano.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa nchi hiyo ilikuwa ikisubiri kwa hamu kumalizika kwa mazungumzo nchini Qatar kati ya maafisa wa DRC na wawakilishi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe na mwenzake wa Congo Therese Kayikwamba Wagner walitia saini mkataba huo mjini Washington nchini Marekani Juni 27.

Rais wa Marekani Donald Trump baadaye alisema Kagame na Rais wa DRC Felix Tshisekedi watakutana hivi karibuni katika Ikulu ya Marekani kutia saini makubaliano ya mwisho ya amani.

Share This Article