Idara ya Mahakama imelalamikia vikali shutuma zinazoelekezewa majaji wanapotoa dhamana katika kesi wanazosikiliza.
Msajili Mkuu wa Idara hiyo ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Huduma, JSC za Mahakama Winfridah Mokaya ametoa mfano shutuma walizoelekezewa majaji katika mahakama za Nanyuki na Kahawa.
“JSC inaelezea mashaka makubwa juu ya visa vinavyooengezeka vya kushambuliwa kwa maafisa wa Idara ya Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yao,” alisema Mokaya kwenye taarifa leo Alhamisi.
“Mienendo kama hiyo inawakilisha visivyo wajibu wa kikatiba wa Idara ya Mahakama, unadhoofisha uhuru wa idara hiyo na kuathiri imani ya umma katika utekelezaji wa sheria kama msingi wa jamii yetu ya demokrasia.”
Mokaya alisisitiza kuwa vigezo mbalimbali huzingatiwa katika utoaji wa dhamana ikiwa ni pamoja na kuzingatia katiba, kanuni ya utaratibu wa uhalifu na miongozo ya dhamana ya Idara ya Mahakama.
Ameapa kuwa idara hiyo haitayumba katika kutoa maamuzi huru katika utenda kazi wake.