Washukiwa wanane wanaohusishwa na uteketezaji wa kituo kwa polisi cha Mawego, kaunti ndogo ya Rachuonyo Kaskazini, kaunti ya Homa Bay wameshtakiwa katika mahakama ya Kahawa kwa ugaidi.
Wanane hao Kennedy Oluoch Oluoch, Nicholas Otieno, Tofiq Owiti Mohamed, Michael Omondi Opiyo, David Bill Clinton Otieno, Robert Ouko Abala, Samuel Ouma Odhiambo na Erick Obunga Osumba, wanadaiwa kutekeleza uhalifu huo Julai 3, 2025.
Washukiwa hao waliokamatwa tena Julai 14, 2025 na kukabidhiwa kwa maafisa wa kitengo cha kukabiliana na ugaidi, walifikishwa katika mahakama ya Kahawa Jumanne na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi, uteketezaji, na uharibifu wa mali.
Walikanusha mashtaka hayo huku upande wa mashtaka ukipinga kuachiliwa kwao kwa dhamana.
Hakimu Mkuu Mwandamizi Richard Koech, alisema kesi ya kuachiliwa kwao kwa dhamana itasikizwa Julai 22, 2025.
Kwa sasa, washukiwa hao wanazuiliwa katika Gereza Kuu la Kamiti.