Serikali imetangaza mipango ya kuzindua Soko la Jumuiya mjini Kisumu ili kuimarisha biashara ya kuvuka mpaka ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.
Hatua hiyo aidha inalenga kuunganisha wafanyabiashara wa eneo hilo na soko pana la kikanda.
Katibu wa Masuala ya EAC Dkt. Carolyn Karugu amesema soko hilo linalenga walaji milioni 130 katika jumuiya hiyo na hivyo kuifanya Kisumu kuwa lango la fursa zinazoongezeka za biashara katika kanda hiyo.
Alizungumza hayo alipomtembelea Gavana wa Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o.
Dkt. Karugu alisema EAC kwa sasa inawajibikia asilimia 29 ya jumla ya biashara humu nchini, na kuifanya kuwa juimuiya kubwa zaidi ya kibiashara kwa nchi hii.
“Mamlaka yetu kama Idara ya Serikali ni kupanua nafasi hii ya biashara ili tusihofu tu juu ya masoko nchini China na Ulaya, wakati ambapo tuna soko ambalo tayari linaweza kutumika hapa katika Afrika Mashariki,” aliongeza Dkt. Karugu.
Taarifa ya KNA