Makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uwazi na uwajibikaji katika utendakazi wao.
Wito huo umetolewa na Mabalozi 11 wanaowakilisha nchi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Denmark, Ireland, Australia na Uswizi.
Mabalozi wengine ni kutoka nchi za Norway, Canada, Uswidi na Ufini.
“Tuna imani kwamba Makamishna wapya watatekeleza majukumu yao bila upendeleo, kwa uwazi, na utaalam katika kuwahudumia Wakenya wote,” walisema Mabalozi hao kwenye taarifa leo Jumanne.
“Tukitazamia mbele, tunalitia moyo Bunge la Taifa na Wizara ya Fedha kuipatia IEBC fedha za kutosha kwa wakati unaofaa, ambazo ni muhimu katika utendakazi wake huru na fanisi.”
Aidha, Mabalozi hao wamezitaka taasisi husika kuchukua hatua muhimu kuhakikisha raia wote wanaostahiki wanajiandikisha kama wapiga kura na kushiriki michakato ya uchaguzi.
Wameelezea utayari wao wa kushirikiana na taasisi husika kuboresha mifumo ya uchaguzi na kuimarisha imani ya Wakenya katika taasisi za umma nchini.
Taarifa yao inakuja siku chache baada ya IEBC kupata Makamishna wapya baada ya kipindi kirefu cha ngoja ngoja.
Walioapishwa kuhudumu kama Makamishna wa tume hiyo ni Erastus Edung Ethekon ambaye atahudumu kama Mwenyekiti huku Kamishna Fahima Araphat Abdallah akiteuliwa kuhudumu kama Naibu Mwenyekiti.
Makamishna wengine ni Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan na Francis Odhiambo Aduol.