Tuko tayari kuandaa CHAN, asema Mvurya

Kenya itaandaa mechi zote nne za Harambee Stars dhidi ya DR Congo, Morocco, Zambia na Angola pamoja na mchuano wa fainali Agosti 30 katika uwanja wa Kasarani.

Dismas Otuke
1 Min Read

Waziri wa Michezo Salim Mvurya amesema Kenya iko tayari kuandaa kipute cha CHAN kati ya Agosti 2 na 30 mwaka huu. 

Mashindano hayo yataandaliwa katika viwanja vya Nyayo na Kasarani.

Mvurya amesema kuwa matayarisho yote yamekamilika kwa fainali hizo, ikiwemo usalama, usafiri na viwanja.

Aidha, Waziri amesema mashindano hayo ya CHAN yanatoa fursa nzuri kwa Kenya kuboresha miundombinu na fursa za kiuchumi.

“Nataka kuhakikishia Wakenya kwamba tumewekeza kabisa katika miundombinu. Uwanja wa Kasarani una mabadiliko makubwa. Miundombinu imewiana na vile vigezo vya CAF kuhakikisha tunaatimiza viwango,”amesema Mvurya.

Waziri aliyasema hayo mapema leo Jumanne kwenye mahojiano ya moja kwa moja kupitia runinga ya KBC Channel 1 na Radio Taifa.

“Mashindano ya CHAN yametupa nafasi ya kujenga miundombinu. Mbali na ujenzi wa viwanja, serikali ya Kenya imelipa ada ya kuandaa mashindano hayo na gharama zingine,” alisisitiza Waziri Mvurya.

Kenya itaandaa mechi zote nne za Harambee Stars dhidi ya DR Congo, Morocco, Zambia na Angola pamoja na mchuano wa fainali Agosti 30 katika uwanja wa Kasarani.

Mechi nyingine za kundi A zitapigwa katika uga wa Nyayo.

Mechi zote 42 za dimba hilo zitarushwa mubashara na runinga ya KBC Channel 1.

Share This Article