Shirika la Kitaifa la Takwimu nchini, KNBS limetuhumiwa kwa kupendelea jamii 5 pekee katika utoaji wa nafasi za ajira.
Kamati ya Kitaifa juu ya Uwiano wa Taifa, Fursa Sawa na Utangamano wa Kikanda ya Seneti imelalamikia hali hiyo ikisema inakiuka katiba ya mwaka 2010 inayotaka kuwepo kwa fursa sawa za ajira katika mashirika ya serikali.
Kulingana na kamati hiyo, ni jamii 5 tu nchini zilizochukua asilimia 64 ya ajira katika KNBS kinyume cha miongozo iliyowekwa na katiba.
Mkurugenzi Mkuu wa KNBS Dkt. Macdonald George Obudho alikuwa na wakati mgumu alipofika mbele ya kamati hiyo leo Jumatatu kuelezea ni kwa nini jamii 5 tu zimependelewa katika nafasi za ajira kwenye shirika hilo.
Hususan, alitakiwa kuelezea ni kwa nini jamii zizo hizo zilipendelewa katika utoaji wa nafasi za ajira wa hivi karibun katika shirika hilo.
Shirika hilo lina wafanyakazi 506 huku 102 wakiwa kutoka jamii ya Kikuyu, 84 Luo, Luhya 60, Kamba 58 na 50 Kalenjin na kufanya kuwa jumla ya 354 idadi ya wafanyakazi kutoka jamii hizo tano wanaohudumu katika shirika hilo.
Isitoshe, asilimia 42.1 ya wafanyakazi walioajiriwa na shirika hilo hivi karibuni walikuwa kutoka jamii hizo tano.
Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta Mohammed Chute ikibaini kuwa KNBS ina wafanyakazi 6 ambao wamepitisha umri wa kustaafu wa miaka 60.
Kamati hiyo imelalamika kuwa vijana wengi wamenyimwa fursa ya kufanya kazi katika shirika hilo licha kuwa na ujuzi unaostahiki.
Dkt. Obudho ameagizwa kuwasilisha nyaraka zaidi juu ya wasambazaji bidhaa kwenye taasisi hiyo na pia namna ya kukabiliana na uvundo wa upendeleo uliokithiri kwenye shirika hilo.