Uhuru amwomboleza Rais Buhari, asema alihudumu kwa uadilifu

Martin Mwanje
2 Min Read
Muhammadu Buhari - Rais wa zamani wa Nigeria / Picha kwa hisani ya Buhari Sallau

Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta amemwomboleza Rais wa zamani wa Nigeria aliyefariki Muhammadu Buhari akimtaja kama kiongozi aliyelitumikia taifa hilo kwa unyenyekevu na kujitolea mno. 

Kifo cha Buhari, mwenye umri wa miaka 82, kilitangazwa kutokea jana Jumapili wakati akipokea matibabu katika kliniki moja mjini London nchini Uingereza.

“Rais Buhari alikuwa siyo tu nembo ya uthabiti lakini pia ya uadilifu,” alisema Uhuru ambaye ni Rais wa zamani wa awamu ya nne wa Kenya kwenye risala zake za rambirambi.

“Alikuwa na msimamo mkali kwa kanuni zake na daima alitoa kipaumbele kwa maslahi ya Nigeria na Afrika kuliko yake.”

Uhuru akimlimbikizia sifa Buhari kwa mchango wake katika kutoa mwongozo wa usalama na uongozi wa bara la Afrika, na kujitolea kwake kwa uthabiti wa kikanda, umoja na jitihada za kukabiliana na jinamizi la ufisadi.

“Aliamini katika nguvu ya suluhu za Kiafrika kwa matatizo ya Kiafrika na kufanya kazi kwa bidii ya mchwa kuiinua sauti ya Nigeria kwenye jukwaa la dunia,” aliongeza Uhuru.

Buhari aliwahi kufanya ziara ya kitaifa nchini Kenya wakati wa utawala wa Uhuru.

Marehemu Rais huyo wa zamani wa Nigeria anatarajiwa kuzikwa leo Jumatatu katika mji wake wa nyumbani wa Daura katika jimbo la Katsina kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Serikali ya Nigeria imetangaza siku 7 za maombolezo kufuatia kifo cha Buhari.

Share This Article