Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC imetakiwa kudumisha uwazi, usawa na kutoegemea upande wowote kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Wito huo umetolewa na kundi la viongozi wa vijana chini ya mwavuli wa shirika la “Munyiri Africa Foundation.”
Vijana hao, wakizungumza wakati wakiwahutubia wanahabari mjini Ruiru, kaunti ya Kiambu, walisisitiza umuhimu wa kutokuwa na upendeleo na kuwa na utaalam katika utenda kazi wa tume hiyo.
Wakiongozwa na Askofu David Munyiri Thagana ambaye ni kinara wa shirika hilo, vijana hao aidha walilaani wimbi la maandamano yenye vurugu yaliyoshuhudiwa nchini wakionya kuwa kuendelea kufanywa kwa maandamano hayo ni tishio kwa uthabiti wa kijamii na kiuchumi wa nchi hii.
Badala yake waamependekeza kubuniwa kwa jukwaa la mazungumzo linaloleta pamoja wadau mbalimbali ili kuangazia changamoto zinazoikumba nchi.
Kinara wa ODM Raila Odinga ametoa pendekezo sawia, pendekezo ambalo limeonekana kupuuziliwa mbali na viongozi wa upinzani na vijana wa Gen Z.
Wito wa uwazi kwa IEBC unakuja siku chache baada ya makamishna wapya wa tume hiyo kuapishwa wiki jana katika hafla iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Walioapishwa wakati wa hafla hiyo ni Erastus Edung Ethekon atakayehudumu kama mwenyekiti mpya wa IEBC huku Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol na Fahima Araphat Abdallah wakila kiapo cha kuhudumu kama Makamishna wa tume hiyo.