Mwakilishi wa Papa wa Kanisa Katoliki humu nchini Maria Van Megen amekashifu uharibifu na wizi wa mali ulioshuhudiwa wakati wa maandamano ambayo yamekuwa kifanyika nchini katika siku za hivi karibuni.
Akizungumza katika kaunti ya Muranga wakati wa maadhimisho ya siku ya elimu katika Dayosisi Katoliki ya Muranga, Megen amesema kuwa ingawa katiba inaruhusu maandamano ya amani, hakuna haki ya kuharibu mali na vile vile kuzua vurugu wakati wa maandamano.
Amesikitika kuwa maandamano ambayo yameshuhudiwa nchini katika siku za hivi karibuni yalisababisha uharibifu mkubwa wa mali na hata vifo vya waandamanaji.
Aidha, Megen amesema itakuwa bora serikali kuwa na mazungumzo na vijana wa kizazi cha Gen-Z ili kujua mahitaji yao, huku akihimiza vijana kukubali kusikiliza serikali ili kutafuta suluhu ya mambo yaliyowaghadhibisha.