Rais William Ruto ametuma salamu za rambirambi kwa watu wa Nigeria kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, akitaja kifo hicho kuwa pigo kubwa kwa Bara la Afrika.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Rais Ruto alimtaja Buhari kuwa kiongozi mwenye busara, uadilifu, na ari ya dhati kwa ustawi wa Afrika.
Kulingana naye, Buhari alicha mchango mkubwa unaoendelea kuhisiwa kote barani. “Kifo cha Rais Buhari ni hasara sio tu kwa watu wa Nigeria bali pia kwa bara zima la Afrika,” alisema Ruto.
Alimsifu Buhari kwa uongozi wake katika kupambana na ufisadi, kuimarisha usalama wa kikanda, na kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.
Ruto pia alikumbuka ziara ya kitaifa ya Buhari nchini Kenya mwaka 2016, akisema ilidumisha na kuimarisha uhusiano kati ya mataifa haya mawili.
Rais wa Kenya alikumbuka kwa upendo ujumbe wa pongezi kutoka kwa Buhari baada ya ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa 2022, akisema ulikuwa ishara ya imani ya Buhari katika demokrasia na umoja wa Afrika.
“Tunapoomboleza na ndugu zetu wa Nigeria, tunaheshimu urithi wake ambao utaendelea kuhamasisha amani, heshima na ustawi wa pamoja barani Afrika” alisema Ruto.
Rais Ruto alisisitiza mshikamano wa Kenya na Nigeria katika kipindi hiki cha maombolezo na kutoa heshima za juu kwa kiongozi huyo wa zamani.