Nicki Minaj ambaye ni mwanamuziki tajika wa Marekani amenyamazisha wakosoaji ambao walitilia shaka uwezo wake wa sasa kifedha kwa kuonyesha maisha anayoishi ya kifahari.
Mwanamuziki huyo wa mtindo wa Rap allitumia akaunti yake ya mtandao wa X, kukanusha madai yaliyosambaa kwamba amefilisika kufuatia maneno aliyomtupia mwanamuziki mwenza Jay-Z na kampuni ya muziki ya Roc Nation.
Minaj alitangaza kwamba yuko katika harakati za kununua jumba lake la tatu katika muda wa miaka miwili tu, akiongeza kwamba amekuwa akinunulia watu wengine mali kwa miaka 15 iliyopita.
Katika chapisho hilo, Minaj alifichua kwamba amenunua ndege ya kibinafsi ya rangi ya waridi au ukipenda Pinki.
Kujionyesha huko mitandaoni kulijiri baada ya Minaj kumlaumu Jay-Z kwa kukosa kumlipa pesa zake dola milioni 200 zilizotokana na mauzo ya hisa za kampuni ya Tidal kwa Square Inc mwaka 2021.
Hatua ya Minaj ya kudai Jay Z pesa hizo hadharani ziliwafanya wengi kudhania kwamba amefilisika ndio maana anazifuatilia.
Msanii huyo anasisitiza kwamba yuko imara kifedha akisema, “Iwapo kesho nitaamka nikiwa na hitahi la Dola milioni 20 hadi 30 cha kufanya ni kupeana albamu yangu. Baadaye nitafanya ziara na kurejesha pesa hizo ndani ya muda mfupi”.
Jay-Z alionekana kutoguswa na mashambulio ya Nicki Minaj mitandaoni alipohudhuria fainali ya mashindano ya kombe la FIFA la Vilabu mwaka 2025 huko New Jersey.
Alichapisha picha za pamoja na mchezaji nyota wa Real Madrid Vinicius Junior ambapo mashabiki wake walitambua kwamba maisha yake yako shwari huku Minaj akimmiminia maneno makali mitandaoni.