Trump akubali rasmi mwaliko wa Mfalme Charles

Trump ataambatana na mkewe Melania Trump, kwa ziara hiyo itakayoanza tarehe 17 hadi 19 Septemba.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais Donald Trump wa Marekani amekubali rasmi mwaliko kutoka kwa Mfalme Charles III kujiunga naye na Malkia Camilla kwa ziara ya kitaifa isiyo ya kawaida kwa mara ya pili, haya ni kulingana na ikulu ya Buckingham.

Rais wa Marekani ataambatana na mkewe, Mama wa Taifa Melania Trump, kwa ziara hiyo itakayoanza tarehe 17 hadi 19 Septemba, na watakaribishwa katika Kasri la Windsor.

Mahali pa kufanyikia ziara hiyo ya kitaifa lilichaguliwa kuwa Kasri la Windsor kwa sababu ikulu ya Buckingham, ambayo kawaida hutumika kwa hafla kama hizo, bado inakarabatiwa.

Trump alikaribishwa na Malkia Elizabeth II kwa ziara yake ya kwanza ya kitaifa mwaka 2019 alipokuwa katika muhula wake wa kwanza wa urais.

Kawaida, marais walioko katika muhula wao wa pili hawapati mwaliko wa ziara ya kitaifa, bali hualikwa kwa chai au chakula cha mchana na mfalme.

Ratiba kamili ya matukio bado haijatangazwa, lakini kama ilivyo kwa ziara zote za aina hii, itajumuisha mapokezi ya heshima kwa sherehe kamili na karamu ya kitaifa katika Ukumbi wa St George ndani ya Kasri la Windsor.

Wanachama wote waandamizi wa Familia ya Kifalme watahusika, wakiwemo Mwana wa Mfalme na Mkewe (Prince and Princess of Wales), ambao wanaishi ndani ya eneo la kasri hilo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikaribishwa na Mfalme katika Kasri la Windsor wiki iliyopita, na hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa ziara ya kitaifa kufanyika katika makaazi hayo ya Berkshire kwa zaidi ya muongo mmoja.

Macron na mkewe, Brigitte, pia walishiriki katika maandamano ya magari ya kifahari yaliyopita katika mji wa Windsor.

Ziara yoyote kutoka kwa Rais wa Marekani huambatana na changamoto za kiusalama, na inaaminika kwamba ratiba ya Trump haitajumuisha matukio ya hadharani.

Wakati wa ziara yake ya mwaka 2019, hakukuwa na maandamano ya kifalme kwenye The Mall kwa sababu za kiusalama, na Trump alisafirishwa kwa helikopta kati ya maeneo mbalimbali badala ya kutumia barabara.

Share This Article