Mchekeshaji wa Tanzania Lucas Mhuvile maarufu kama Joti amepata heshima ya kuwa Mchekeshaji Bora wa Mwaka 2024 katika tuzo za HAPA Awards.
Joti amekuwa mstari wa mbele katika sekta ya ucheshi, akiwaletea wengi furaha na tabasamu kupitia vipindi vyake vya vichekesho.
Tuzo hii ni thibitisho la mchango mkubwa wa Joti katika kukuza na kuendeleza sanaa ya ucheshi nchini Tanzania, huku akiwahamasisha wachekeshaji wengine kufanikisha kazi zao kwa ubunifu na ubora.
Hafla rasmi ya kutoa tuzo za HAPA yaani Hollywood & African Prestigious Awards za mwaka 2024 iliandaliwa Oktoba 27, 2024 katika ukumbi wa maonyesho wa Wilshire Ebell, huko Los Angeles nchini Marekani.
Kilichofanyika jana Julai 12, 2025 katika hoteli ya Landmark jijini Dar es Salaam, ni kuwasilishia washindi wa Tanzania tuzo zao za wakati huo.
Hafla hiyo ya jana ilihudhuriwa na wasanii wa muziki na filamu, viongozi wa serikali, watu maarufu na wadau wa sanaa na utamaduni.
Wengine waliopokea tuzo zao ni pamoja na Jacob Stephen Mbura maarufu kama JB wa Jerusalem Films ambaye ni mwigizaji na mwandalizi wa filamu nchini Tanzania.
JB ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya filamu nchini Tanzania, alipokea tuzo ya nyota mkuu katika sekta ya burudani kwa kutambua mchango wake mkubwa na uongozi bora katika kukuza filamu na burudani Tanzania.