AgaNaga aonya dhidi ya kuhusisha wanamuziki katika siasa

Anashauri wasanii wanaounga mkono Bobi Wine kukoma kumwigiza hasa katika matamshi na vitendo vya kisiasa.

Marion Bosire
1 Min Read
Kalifah AgaNaga

Mwanamuziki wa Uganda Sadat Mukiibi maarufu kama Kalifah AgaNaga amewataka raia wa Uganda hasa wanaounga mkono chama kikuu cha upinzani National Unity Platform – NUP wakome kuhusisha wanamuziki katika masuala fulani ya kisiasa nchini humo.

Katika ujumbe huo aliowasilisha kupitia video, Kalifah alisema kwamba wafuasi wengi na hata washawishi wa mitandaoni huchukulia wanamuziki wa kawaida kuwa kama Bobi Wine.

Alisisitiza kwamba Bobi Wine yuko katika kiwango cha Urais, ligi aliyotaja kuwa muhimu, na inampa uhuru wa kutoa maoni yake bila woga wa yatakayomtokea.

“Ninataka kusema kwamba Bobi Wine anasimama katika kiwango chake peke yake ndiyo maana anaweza kuchukua hatua zozote apendavyo,” alisema AgaNaga.

Akiongeza kwamba Wine hushughulikia mambo kwa njia ya kirais na yeye huchukuliwa kama kiongozi wa ligi ya juu.

“Bobi Wine anapofanya mambo na kuzungumza kwa namna fulani, hiyo haikupi fursa ya kumuiga. Kujaribu kufanya hivyo kunaweza kukusababishia madhara kwa sababu wewe sio wa kiwango sawa na Wine,” alishauri mwanamuziki huyo.

Msanii huyo sasa anashauri wanamuziki washughulikie tu masuala yaliyo ndani ya uwezo wao badala ya kujihusisha na yale yaliyowazidi.

Kalifah alisema Bobi Wine ana wanamuziki anaoshirikiana nao ba atawaita wakati atahitaji usaidizi wao.

Share This Article