Makamishna wapya wa IEBC waapishwa

Martin Mwanje
3 Min Read
Erastus Edung Ethekon - Mwenyekiti mpya wa IEBC

Sasa ni rasmi kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ina makamishna wapya.

Hii ni baada ya Jaji Mkuu Martha Koome kuongoza hafla ya uapisho wa Erastus Edung Ethekon kuapishwa kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo katika hafla iliyofanyika katika afisi za Mahakama ya Juu jijini Nairobi leo Ijumaa.

Wakati wa hafla hiyo, Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol na Fahima Araphat Abdallah walikula kiapo cha kuhudumu kama Makamishna wa tume hiyo.

Punde baada ya kula kiapo, Ethekon aliahidi Wakenya kwamba IEBC itafanya kila iwezalo kusimamia uchaguzi huru na wa haki humu nchini siku zijazo.

Aliwaomba Wakenya kuunga mkono makamishna wapya wa tume hiyo wanapovalia njuga kuhakikisha utenda kazi wa tume hiyo ni wa kupigiwa mfano.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Martha Koome alitoa wito kwa makamishna wapya wa IEBC kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa njia huru bila kushurutishwa na mtu yeyote.

Kwa kufanya hivyo, Jaji Koome alisema makamishna hao watafanikiwa kurejesha imani ya raia kwenye tume hiyo wakati ambapo imani ya Wakenya katika taasisi za umma imekuwa ikididimia.

“Mnachukua madaraka wakati wa tafakari ya taifa – kipindi ambapo Wakenya, hasa vijana, wanaelezea kutoridhishwa kwao na taasisi za umma. Nchi ina kiu ya uadilifu, uwazi, uwajibikaji, na haki,” alisema Jaji Mkuu kwenye hotuba yake.

“Ni kwa misingi hii ambapo mamlaka yenu yana hata umuhimu mkubwa zaidi. Demokrasia yetu ni lazima ijikite kwa msingi thabiti, na sasa nyinyi ndio waongozaji wa msingi huo.”

Makamishna wapya wa IEBC walikula kiapo cha utenda kazi siku moja baada ya wao kuteuliwa upya na Rais William Ruto kupitia gazeti rasmi la serikali.

Hii ni baada ya kesi iliyokuwa imewasilishwa mahakamani kupinga uteuzi wao kutupiliwa mbali.

Kwenye uamuzi uliotolewa jana Alhamisi alasiri, Majaji wa Mahakama Kuu waliharamisha ilani ya gazeti rasmi la serikali toleo la Juni 10, 2025 iliyowateua makamishna hao, kwa misingi kuwa mahakama ilikuwa imetoa maagizo kwamba makamishna hao wasichapishwe kwenye gazeti rasmi la serikali.

Ethekon na kikosi chake wanachukua hatamu za uongozi wa IEBC wakifahamu kwamba kibarua cha kufanya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 kitakuwa cha kukuna kichwa ikizingatiwa muda unayoyoma.

Kisha kuna chaguzi kadhaa ndogo zinazopaswa kufanywa yamkini haraka iwezekanavyo, kwani baadhi ya maeneo yamekosa uwakilishi bungeni kwa muda mrefu.

Share This Article