Mwanamuziki wa Uganda King Saha ameapa kuhakikisha kwamba miziki ya wasanii wa asili ya Uganda inapata kuchezwa zaidi kwenye vyombo vya habari na maeneo ya burudani nchini humo.
Kulingana naye wakati umewadia kwa talanta za nyumbani kutawala, baada ya miziki ya nchi nyingine hasa Nigeria kupendelewa zaidi.
Akizungumza kwenye TikTok Live ambapo alikuwa na A Pass, King Saha alisema kwamba wanamuziki wa Uganda wana uwezo wa kurejesha umakini wa wasikilizaji wao kutoka kwa miziki ya Nigeria.
Msanii huyo ambaye amepeleka burudani huko Dubai kwa sasa anasema wasanii hao wanaweza kufurahisha wasikilizaji wa nyumbani kwa sauti nzuri na midundo ya kipekee.
“Wakati umewadia kwa miziki mizuri kama yangu kuteka anga zaidi ya miziki ya Nigeria ambayo imekaba wasikilizaji wa Uganda,” alisema msanii huyo.
King Saha hata hivyo aliwasifia wasanii wa muziki wa Nigeria kwa mbinu zao za kimkakati za kutumia densi kuburudisha mashabiki, akisema wameweza kubadili midundo hata ya kawaida kuwa mitindo ya denso inayopendwa sana.
“Wanamuziki wa Nigeria waliangazia mitindo ya densi kama Eddy Kenzo. Kila unapotoa muziki wanaanza tu kucheza,” alisema msanii huyo akiongeza kwamba msanii anapogundua mapungufu yake anapaswa kutafuta namna ya kuyafunika.