Mradi wa mwanamuziki Akon wa jiji la Akon nchini Senegal umekomeshwa na serikali ya nchi hiyo ambayo sasa imechukua tena usimamizi wa eneo lililokuwa limetengewa ujenzi huo.
Hii ni baada ya msanii huyo tajika kushindwa kukamilisha mradi huo kulingana na makubaliano kati yake na serikali ya Senegal.
Alikuwa amepanga kujenga mji huo kwa namna sawa na miji ambayo ilionyeshwa kwenye filamu ya Black Panther lakini ameshindwa na serikali ya Senegal sasa imefuta mradi huo.
Inaripotiwa kwamba serikali hiyo sasa inapanga kuwekeza dola bilioni 1.2 katika eneo hilo ambapo itajenga hoteli na nyumba za kupanga kwa ajili ya watalii kwani eneo hilo liko karibu na fukwe.
Akon alikuwa amepatiwa eneo la ukubwa wa ekari 136 na serikali ya Senegal mwaka 2020 kwa ajili ya kujenga Akon City, jiji ambalo lingebadilisha Mbodiène kutoka Kijiji cha wakulima na kuwa Jiji la kisasa kwa gharama ya dola bilioni 6.
Awamu ya kwanza ya mradi huo ilitarajiwa kukamilika mwaka 2023.
Mwezi Agosti mwaka jana serikali ya Senegal ilimkumbusha Akon kuhusu ujenzi wa mradi huo huku aneo husika likibadilishwa kuwa malisho ya mifugo.
Akon alizaliwa nchini Marekani lakini wazazi wake ni wa asili ya Senegal.