Jamii ya Waislamu humu nchini inaomboleza kufuatia kifo cha Kadhi Mkuu, Sheikh AbdulHalim Hussein.
Sheikh Hussein aliripotiwa kufariki akiwa nyumbani kwake jijini Mombasa jana Jumatano usiku.
Ripoti zake zilitangazwa kupitia mtandao wa X na Imamu wa msikiti wa Jamia, Sheikh Jamaludin Osman.
Amepangiwa kuzikwa leo Alhamisi baada ya swala ya alasiri.
Kifo chake kinahitimisha muda wake wa kuhudumu kama mkuu wa mahakama za Kadhi nchini.
Sheikh Hussein aliteuliwa kuwa Kadhi Mkuu wa Kenya mwezi Julai mwaka wa 2023 baada ya mchakato wa uajiri ulioongozwa na Tume ya Huduma za Mahakama.
Alichaguliwa miongoni mwa wagombeaji watano walioorodheshwa kumrithi Sheikh Ahmed Muhdhar, ambaye alistaafu baada ya kuhudumu kwenye wadhifa huo kwa kipindi cha miaka 12.
Aidha, Sheikh Muhdar alikuwa amefikisha umri wa miaka 60 wakati wa kuondoka kwake kwenye wadhifa huo.
Jaji Mkuu Martha Koome ameomboleza kifo cha Sheikh Hussein akimtaja kuwa Kadhi aliyewahudumia Wakenya kwa kujituma, unyenyekevu na uadilifu.
“Kama Kadhi Mkuu, alikuwa mtetezi wa haki na usawa, hasa katika masuala ya sheria ya kibinafsi ndani ya jamii ya Waislamu,” alisema Jaji Koome kwenye risala zake za rambirambi.
Kadhi Mkuu Hussein ataswaliwa baadal asri masjid Nuru Bondeni na kuzikwa maziara ya Kikowani upande wa Seif Halwa.