Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy leo Jumatano amekutana na Papa Leo wa 14, mkesha wa mkutano wa kimataifa utakaofanyika mjini Roma juu ya ujenzi mpya wa nchi yake inayokumbwa na vita.
Zelenskyy pia alipangiwa kukutana na Rais wa Italia Sergio Mattarella na Keith Kellogg, ambaye ni mjumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu masuala ya Ukraine na Urusi, kwa mujibu wa afisi ya Rais ya Ukraine.
Mkutano na Papa ulikuwa wa pili wa faragha kati yao tangu Papa Leo kuchaguliwa kuongoza Kanisa Katoliki duniani.
Papa Leo ni Mmarekani wa kwanza kuwahi kuliongoza kanisa hilo.
Mkutano kati yao ulifanyika katika makazi ya msimu wa joto ya Papa Leo huko Castel Gandolfo, yanayopatikana kwenye ziwa kusini mwa mji mkuu huo wa Italia anakokaa Papa Leo kwa kipindi cha wiki mbili hadi Julai 20.
Zelenskyy yuko mjini Roma kushiriki Mkutano wa Ujenzi Mpya wa Ukraine, mkutano wa kimataifa wa siku mbili uliopangwa kufanyika kesho Alhamisi na Ijumaa.
Lengo la mkutano huo ni kutafuta uungwaji mkono, ikiwa ni pamoja na uwekezaji wa kibinafsi, kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukraine.
Viongozi, akiwemo Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, wanatarajiwa kuhudhuria sambamba na wawakilishi kutoka kwenye takriban kampuni 2,000 na mashirika 40 ya kimataifa, kwa mujibu wa mwenyeji wa mkutano huo, Italia.