Gaetano kupanga mkutano wa wahusika wa BBA ya kwanza

Kaggwa anahisi itakuwa furaha ya aina yake wawaniaji hao wa mwaka 2003 wa Big Brother Africa wakikutana tena baada ya miaka 22.

Marion Bosire
2 Min Read

Mtangazaji wa redio nchini Uganda Gaetano Kaggwa ametangaza mpango wa kuandaa mkutano wa wahusika wa kwanza kabisa wa kipindi cha runinga cha Big Brother Africa cha mwaka 2003.

Kaggwa anasema anaendeleza kuhudi za kuwasiliana na wahusika wote 12 waliowakilisha nchi 12 za Afrika katika makala hayo akisema wengi walichagua tasnia tofauti maishani.

Njia aliyochagua Kaggwa ya utangazaji wa redio, inasadifiana na aliyochagua mwakilishi wa Kenya katika makala hayo ya mwaka 2003 ya BBA Sheila Kwamboka maarufu kama Kwambox.

Makala ya kwanza kabisa ya Big Brother Africa, kipindi ambacho baadaye kilifuatiliwa na wengi ndani na nje ya Afrika, yaliandaliwa kwa siku 106, kati ya Mei 25, 2003 na Septemba 7, 2003.

Mtangazaji wa makala hayo alikuwa Mark Pilgrim wa Afrika Kusini ambapo makala hayo yaliandaliwa.

Angola iliwakilishwa na Bruna Estivao, Botswana ikawakilishwa na Warona Masego Setshwaelo, Ghana ikawakilishwa na Samuel Kwame Bampoe, Kenya iliwakilishwa na Sheila Kwamboka, Malawi ikawakilishwa na Zein Dudha huku Namibia ikiwakilishwa na Stefan Ludik.

Nigeria, Africa Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe ziliwakilishwa na Alexander Adebayo Adetomiwa Okoh, Abergail Brigette Plaatjies,Mwisho Mwampamba, Gaetano Kaggwa, Cherise Makubale na Tapuwa Mhere mtawalia.

Watazamaji walipata fursa ya kujionea haiba tofauti pamoja na utamaduni wa mataifa mbali mbali ya bara hili la Afrika.

Cherise Makubale wa Zambia ndiye aliibuka mshindi wa makala hayo.

Share This Article