Gavana wa kaunti ya Isiolo Abdi Guyo amenusurika kutimuliwa baada ya Seneti kuamua kwamba Bunge la kaunti ya Isiolo halikufuata utaratibu ufaao kumuondoa mamlakani.
Kulingana na Seneti iliyoandaa kikao cha kusikiliza hoja ya kutimuliwa kwa Gavana huyo siku ya Jumanne, Bunge la kaunti ya Isiolo halikuandaa kikao cha kujadili na kupigia kura hoja ya kumuondoa mamlakani Gavana huyo.
Maseneta 31 walipiga kura kumnusuru Gavana huyo huku 11 wakiunga mkono kutimuliwa kwake.
“Bunge la Seneti limegundua kwamba Bunge la kaunti ya Isiolo halikuandaa vikao Juni 18, 2025 na Juni 26, 2025 kusikiliza na kupigia kura hoja ya kumuondoa afisini Gavana wa kaunti ya Isiolo, Abdi Hassan,”ilisema taarifa ya Seneti.
Maseneta walishiriki vikao maalum siku ya Jumanne kusikiliza hoja ya kumuondoa madarakani Gavana Guyo ambaye aliwakilishwa na kundi la mawakili wanane wakiongozwa na Elisha Ongoya na mashahidi watano, huku bunge la kaunti ya Isiolo likiongozwa na kundi la mawakili 10 na mashahidi wanne.
Bunge lote la Seneti lilisikiliza hoja hiyo, baada ya kukatalia mbali pendekezo la kubuniwa kwa kamati ya wanachama 11 kuchunguza madai dhidi ya Gavana Guyo.
Gavana Guyo aliondolewa mamlakani na Bunge la kaunti ya Isiolo kwa madai ya utumizi mbaya wa mamlaka, ukiukaji wa katiba na ukosefu wa maadili.
Wanachama 18 wa Bunge la Kaunti ya Isiolo walipiga kura kumtimua Gavana Guyo Juni 26, 2025.