Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo, ametoa wito kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kutuma kundi la maafisa wa upelelezi, kuchunguza visa vya mauaji vinayowalenga wasichana wadogo katika eneo bunge hilo.
Akizungumza katika eneo la Mutumbu, kaunti ndogo ya Yala, mbunge huyo alieleza kuwa idadi inayoongezeka ya mauaji hayo, imesababisha hofu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
“Inasikitisha kuwa wasichana wadogo na wakazi wanakuwa waathiriwa wa mauaji hayo ambayo labda yanatekelezwa na mtu au genge la majambazi,” alisema mbunge huyo.
Matamshi ya mbunge huyo yamejiri kufuatia mauaji ya mjane Veronica Odongo na Elizabeth Achieng, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili, ambao waliuawa siku tatu zilizopita. Miezi miwili awali, wanafunzi wawili waliuawa katika eneo la Mindhine na Muhanda.
“Hatuwezi endelea hivi. Natoa wito kwa kila mmoja wetu kutoa taarifa kwa polisi zinazohakikisha watu wetu wanalindwa,” aliongeza Odhiambo.
Alitaja Sagam, Sinaga, na East Mashariki kuwa hatari zaidi kwa shughuli za uhalifu.