Raila: Mazungumzo ya kitaifa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi

Tom Mathinji
1 Min Read
Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga akiwahutubia wanahabari kuhusu maandamano ya Saba Saba.

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, ametoa wito wa Kongamano shirikishi la kitaifa ambalo litawasikiliza Wakenya wote kwa lengo la kutatua changamoto zinazoghubika taifa hili, ili kuhakikisha linasonga mbele.

Akizungumza Jumatatu kuadhimisha miaka 35 ya Maandamano ya Saba Saba, Raila alisema mazungumzo hayo yatafanikisha kuwasikiliza wakenya wote ili kuleta mageuzi yatakayoimarisha uongozi wa taifa hili.

Kwenye hotuba hiyo aliyoitoa akiwa katika hoteli moja Jijini Nairobi, Raila alisema matokeo ya mazungumzo hayo yanapaswa kuidhinishwa kupitia kura ya maamuzi, kutoa fursa kwa wakenya kuamua mustakabal wa nchi hii.

“Ninapendekeza kongamano la kitaifa  litakaloshirikisha wote ili kuwasikiliza watu wa tabaka mbali mbali na kubuni mageuzi yatakayopeleka taifa hili mbele,”alisema Raila.

Kiongozi huyo wa ODM, alisema Wakenya wanataka sheria zinazowajibisha taasisi kuitikia mipango inayohakikisha ufadhili wa kutosha kwa huduma zinazofungamana na mahitaji yao na mahakama huru.

Kuhusu maandamano ya Saba saba ambayo yalifanyika Julai 7,1990, Raila alisema lengo lake lilikuwa kupigania uhuru, usawa na mageuzi ya katiba bila kujali miegemeo ya kisiasa, kijamii, taaluma au kijamii.

“Saba Saba haikuwa kundi moja dhidi ya taifa, au jamii dhidi ya nyingine, au umri mmoja dhidi ya mwingine. Maandamano hayo yalishinikiza mageuzi ya katiba,”alisema Raila.

Share This Article