Dax Vibez na Mikie Wine wakamatwa

Wawili hao pamoja na wasaidizi wao walikuwa wanatoka kutumbuiza kwenye tamasha la Ekitudha lililoandaliwa na kituo cha runinga cha Baba TV.

Marion Bosire
1 Min Read

Wanamuziki wa Uganda Dax Vibez na Mikie Wine wanaripotiwa kutiwa mbaroni leo alfajiri walipokuwa njiani kutoka Jinja.

Kulingana na ripoti, Mikie Wine na Dax Vibez ambao wote ni ndugu za mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine walikumbana na maafisa wa polisi yapata saa nane alfajiri huko Jinja.

Wawili hao pamoja na wasaidizi wao walikuwa wanatoka kutumbuiza kwenye tamasha la Ekitudha lililoandaliwa na kituo cha runinga cha Baba TV.

Video ya tukio la kukamatwa kwa wawili hao na wasaidizi wao ilisambazwa mitandaoni ambapo Dax Vibez anasikika akipigia mayowe akiomba usaidizi akisema kwamba wanakamatwa bila sababu.

Maafisa wa polisi bado hawajatoa taarifa kuhusu kukamatwa kwa wawili hao.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Dax Vibez kusema kwenye mahojiano kwamba tofauti kati yake na Eddy Kenzo ambaye ni mshauri wa Rais kuhusu wabunifu na Rais wa shirikisho la wanamuziki nchini Uganda UNMF ni za kimaoni na sio za kibinafsi.

Alimlaumu Kenzo kwa kushirikiana na serikali na kukosa kuendeleza maslahi ya wanachama wa UNMF ambao ni wanamuziki.

Share This Article