Rais William Ruto ametetea hatua yake ya kujenga upya kanisa katika Ikulu ya Nairobi, akisema kanisa hilo limekuwepo kwa zaidi ya Karne moja.
Kiongozi wa nchi aliyezungumza katika maadhimisho ya miaka 35 ya Dayosisi ya Embu ya kanisa la ACK, alielezea kwamba kanisa hilo lilikuwa limeanza kuchakaa.
Ruto alisema kwamba jengo hilo likikamilishwa, litahudumia wakazi wapatao 300 wa Ikulu ambao wamekuwa wakitumia jengo hilo la zamani ambalo lingeweza kuporomoka wakati wowote hata wakiendelea na ibada.
Rais alikanusha pia gharama ya ujenzi wa kanisa hilo ambayo imekuwa ikitangazwa akisema gharama halisi ni ndogo zaidi ya hiyo.
Wakati huo huo, viongozi wa kidini wamejitokeza kuunga mkono ujenzi wa kanisa hilo katika Ikulu ya Nairobi, wakisema ni hatua inayofaa.
Wakiongozwa na Wakiongozwa na Askofu Samuel Njiriri wa Kanisa la Stewards Revival Pentecostal, viongozi hao walikashifu wanaopinga uamuzi huo wa Rais wakisema hawana ufahamu.
Njiriri pia alitoa wito wa ustahimilivu wa kisiasa humu nchini kabla ya uchaguzi mkuu ujao akishutumu wanasiasa ambao tayari wako katika hali ya kampeni na wanagawanya Wakenya kwa misingi ya kabila.