Mel B na Rory McPhee wafanya harusi

Harusi ya wawili hao iliandaliwa katika kanisa la Mtakatifu Paulo jijini London jana Jumamosi

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uingereza Melanie Janine Brown maarufu kama Mel B alifunga ndoa na mtaalamu wa masuala ya nywele Rory McPhee katika hafla iliyohudhuriwa na watu maarufu huko London.

Harusi ya wawili hao iliandaliwa katika kanisa la Mtakatifu Paulo jijini London jana Jumamosi ambapo Mel alikuwa amevaa nguo ndefu nyeupe iliyokuwa na shanga iliyoundwa na msanifu wa mitindo ya mavazi Josephine Scott.

Rory kwa upande wake alikuwa amevaa vazi la kitamaduni aina ya Kilt na walionekana wenye furaha na walionyesha upendo uliopo kati yao kwa mabusu baada ya sherehe ya kanisani.

Baada ya hafla ya kanisani, Mel B alibadilisha vazi na kuvaa gauni aliyoshonewa na Justin Alexander.

Hii ndio mara ya tatu Mel B wa umri wa miaka 50 sasa anaolewa. Alikuwa kwenye ndoa awali na mcheza densi Jimmy Gulzar mwaka 1998 hadi 2000 na baadaye akaolewa na Stephen Belafonte mwaka 2007 ndoa iliyodumu miaka kumi hadi mwaka 2017.

Wanawe watatu wa kike walihudumu kama wasaidi wake kwenye harusi yake ya jana.

Mel na Rory walichumbiana mwaka 2022 lakini uhusiano wao wa kimapenzi unaaminika kuanza mwaka 2018.

Share This Article