Wakenya wamehakikishiwa usalama wa chanjo inayotolewa na serikali kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 15 dhidi ya magonjwa ya Surua-Rubella na homa ya matumbo katika mpango ulioanza jana Julai 5 hadi 14, 2025.
Mkurugenzi mkuu wa Afya Patrick Amoth ambaye alikuwa akizungumza katika hafla ya kuzindua utoaji wa chanjo hizo katika uwanja wa Githogoro jijini Nairobi alisema kwamba chanjo hizo huchunguzwa kwa kina kabla ya kutolewa.
Amoth aliwasihi wazazi na watunzaji wa watoto kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hizo akiongeza kusema kwamba kama wizara wamejitolea kulinda afya ya kila mkenya hasa watoto kupitia chanjo salama na yenye ufanisi.
“Chanjo zote zikiwemo za Surua-Rubella na homa ya matumbo, zimepitia mipango ya kina ya uangazili. Kabla chanjo iwekwe katika ratiba ya chanjo ya Kenya, lazima ipitie viwango viwili huru vya uchunguzi.” Alisema Amoth.
Kulingana naye kiwango cha kwanza ni cha kundi la kitaifa la ushauri kuhusu chanjo – KENITAG, ambalo hudurusu deta iliyopo kuhusu usalama, ufanisi na kukubalika kwa chanjo hizo ulimwenguni kote.
Amoth alisisitiza kwamba chanjo ni mojawapo ya njia mwafaka zinazotumiwa katika afya ya umma kuzuia milipuko ya magonjwa, kuokoa maisha na kupunguza gharama ya matibabu.
Katibu wa afya ya umma Mary Muthoni ambaye pia alihudhuria uzinduzi huo alipongeza wahudumu wa afya ya jamii kwa kujitolea kufikia kila mtoto nyumbani kwao.
Ouma Oluga katibu wa huduma za matibabu kwa upande wake alielezea kwamba wamebuni kamati inayojumuisha wawakilishi wa sekta ya usalama wa ndani na elimu kuhakikisha chanjo inafika katika kila shule.