Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, amesema hatawania kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi ujao wa ubunge, na kuhitimisha kipindi cha miaka 15 cha kuwa mbunge.
Aidha hatua hiyo itasababisha kutoteuliwa kwake kwa wadhifa wa Waziri Mkuu wakati wa uchaguzi huo.
Majaliwa awali alisema kuwa atawania tena kiti chake cha ubunge kwa mara ya nne mwezi Oktoba kabla ya kutoa tangazo hilo ambalo halikutarajiwa.
Akizungma wakati wa mkutano na wanachama wa kamati ya kisiasa eneo la Ruangwa siku ya Jumatano, Majaliwa aliwashukuru watu wa eneo bunge lake kutokana na jinsi walivyomuunga mkono wakati wa kipindi hicho alicho shikilia wadhifa wa mbunge.
Aliwahimiza wanachama hao kudumisha umoja na maendeleo.
“Imefika wakati ambapo tunapaswa kutoa fursa kwa wakazi wengine wa Ruangwa kuendeleza mbele kazi tuliyoanzisha,”alisema Majaliwa.
Waziri huyo mkuu mwenye umri wa miaka 64 aliteuliwa kwa wadhifa huo mwaka wa 2015 na alitarajiwa kuchukua nafasi ya hayati aliyekuwa rais wa nchi hiyo, John Magufuli kufuatia kifo chake mwaka 2021.
Amekuwa akishikilia wadhifa huo chini ya rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anatetetea kiti chake cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Majaliwa,ambaye amewakilisha eneo la pwani la Ruangwa tangu mwaka 2010, alisema uamuzi wake unaongozwa na Mola na kwamba alifanya uamuzi huo kwa imani .