Australia yamkataa Kanye West

Visa ya mwanamuziki huyo ya Australia ilifutwa baada yake kutoa wimbo wa kusifu kiongozi wa Nazi, Adolf Hitler.

Marion Bosire
2 Min Read

Taifa la Australia limetangaza kwamba mwanamuziki wa Marekani Kanye West ambaye alibadili jina na kujiita Ye, haruhusiwi kuingia nchini humo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Australia Tony Burke alisema kwamba idara yake imefutilia mbali Visa aliyokuwa nayo mwanamuziki huyo kufuatia wimbo alioimba wa kusifia kiongozi wa Nazi, Adolf Hitler.

Wimbo huo uitwao “Heil Hitler” ambao Ye aliutoa mwanzo wa mwezi Mei mwaka huu wa 2025 umekashifiwa na wengi ulimwenguni kote na kupigwa marufuku na majukwaa kadhaa ya kusambaza muziki.

Ye hujitambulisha kama mwanachama wa Nazi na anafahamika kwa matamshi yake dhidi ya wayahudi.

Waziri Burke alifichua kuzuiwa kwa Kanye kuingia Australia katika mahojiano ambapo alijadili pia kufutwa kwa Visa ya mtu mwingine aliyetoa matamshi mabaya kuhusu dini ya kiisilamu.

Haijulikani iwapo hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ya Australia dhidi ya Kanye ni ya muda au ya kudumu, huku Burke akifafanua kwamba maombi ya Visa ya kuingia nchini humo hurejelewa kila mara kulingana na sheria.

Hii sio mara ya kwanza Kanye anakabiliwa na hali hii nchini Australia, mwaka 2023 waziri wa elimu nchini Australia Jason Clare alilalamikia matamshi ya Kanye kuhusu Hitler na maangamizi makuu na kupendekeza azuiwe kuingia Australia.

Wimbo huo wa Heil Hitler ambao uko kwenye albamu ya WW3, ulitizamwa mara milioni kadhaa katika siku ya kwanza ya kuchapishwa mwezi Mei mwaka huu.

Video ya wimbo huo inaonyesha kundi la wanaume waliovaa ngozi za wanyama wakiimba maneno ya jina la wimbo huo. Baada ya kuutoa, Kanye aitangaza kwamba ameachana na matamshi dhidi ya wayahudi na kutoa wimbo mwingine kwa jina Hallelujah.

Share This Article