Mwanablogu Ndiangui Kinyagia ajitokeza mahakamani

Anasema alikuwa amekwenda mafichoni baada ya kufahamu kwamba maafisa wa upelelezi wa jinai walikuwa wakimsaka.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanablogu aliyekuwa ametoweka Ndiangui Kinyagia amejitokeza katika mahakama kuu leo Alhamisi Julai 3, 2025, baada ya mahakama hiyo kuagiza mkuu wa idara ya upelelezi wa jinai nchini kumwasilisha.

Kinyagia alitoweka kwenye makazi yake ya Kinoo, kaunti ya Kiambu Juni 22, 2025 baada ya kile ambacho majirani walitaja kuwa uvamizi wa maafisa wa upelelezi wa jinai.

Leo alfajiri, wakili wa familia ya mwanablogu huyo aitwaye Wahome Thuku alitangaza kwamba alikuwa amewasiliana na familia yake, akawafahamaisha kwamba yuko salama na akaahidi kufikisha mahakamani.

Kulingana na Thuku, Ndiangui aliwasiliana na mmoja wa watu wa familia yake Jumanne jioni kutoka eneo lisilojulikana akamwambia kwamba alikuwa amejificha baada ya kufahamu kwamba maafisa wa upelelezi walikuwa wakimtafuta.

Awali idara ya upelelezi wa jinai ilikuwa imekanusha kumshikilia mwanablogu huyo ambapo mkurugenzi mkuu Mohammed Amin alifafanua Jumatatu kwamba Kinyagia hakuwa ametiwa mbaroni.

Katika taarifa yake ya Jumatatu alasiri, Amin alikiri kwamba idara hiyo ina shauri na mwanablogu huyo kutokana na machapisho yake kwenye mtandao wa X lakini hawakuwa wamemkamata.

Jumatatu mahakama kuu ilitoa agizo kwa Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, amwasilishe Kinyagia mahakamani Jumanne asubuhi au aelezee aliko.

Kupatikana kwake ni afueni kwa watu wa familia yake waliokuwa na wasiwasi na walioonekana kuzidiwa na hisia walipokuwa wakimpiga pambaja mahakamani leo asubuhi.

Share This Article