Baadhi ya Waislamu wapinga uamuzi wa mahakama kuhusu urithi wa mali

Tom Mathinji
2 Min Read
Sheikh Abu Qatada akizungumza na wanahabari Mombasa.

Baadhi ya viongozi wa kiislamu katika eneo la pwani wamepinga vikali uamuzi wa hivi majuzi wa mahakama ya juu ambao unaruhusu watoto waliozaliwa nje ya ndoa kuridhi mali ya baba zao waisilamu,wakisema uamuzi huo unakiuka sheria za kiislamu na unaingilia kati majukumu ya mahakama za Kadhi.

Wakiongea na wanahabari huko Mombasa,viongozi hao wa kidini walisema uamuzi huo unakiuka uhuru wa kidini na maadili ya kiislamu kuhusiana na urithi.Walitoa wito kwa serikali na taasisi za kisheria kuingilia kati la kulinda utekelezaji wa sheria ya kibinafsi ya kiislamu kuambatana na katiba.

Sheikh Abu Qatada, ambaye ni mwenyekiti wa kongamano la viongozi wazalendo wa kidini huko Pwani,alielezea hisia zake kuhusu uamuzi huo wa mahakama ambao alisema ulipuuza wajibu wa mahakama za kadhi katika utatuzi wa mizozo ya kifamilia miongoni mwa waisilamu.

“Tumeshangazwa na uamuzi wa Mahakama ya Upeo ambao unawaruhusu watoto waliozaliwa nje ya ndoa kurithi mali sawa na wale walio kwenye ndoa. Nchi yetu inatoa fursa ya uhuru wa kuabudu na maswala wa familia huzingatia dini zetu. Tunahimiza mahakama kuacha maswala hayo yashughulikiwe na mahakama za kadhi,”alisema Sheikh Qatada.

Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa tarehe 30 mwezi jana kwenye kesi kati ya Fatuma Athman Abud Faraj  na Ruth Faith Mwawasi.

Mahakama ya Upeo, ilitupilia mbali rufaa iliyotaka kuwatenga watoto waliozaliwa nje ya ndoa kurithi mali chini ya sheria za kiislamu, ikishikilia kuwa hatua hiyo ni ya ubaguzi kinyume na sehemu ya 27 na 53 ya katiba.

Share This Article