Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Mohamed Amin, ametakiwa kufika katika Mahakama Kuu Nairobi siku ya Alhamisi, kuelezea aliko mwanablogu Ndiang’ui Kinyagia.
Akitoa agizo hilo, Jaji Chacha Mwita alisema maafisa kutoka idara hiyo ya upelelezi, walikuwa watu wa mwisho kuzuru nyumbani kwake mwanablogu huyo kabla ya kutoweka kwake.
Jaji Mwita alidokeza kuwa mahakama inataka ufafanuzi kutoka kwa Amin kuhusu aliko mwanablogu Kinyagia, huku akitakiwa na mahakama hiyo lazima awajibikie vitendo vya idara hiyo.
Aidha, Jaji huyo pia aliwaagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, na Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin kumwasilisha mwanablogu huyo akiwa hai au akiwa ameaga dunia. Jaji Mwita alitaka kesi hiyo itajwe Alhamis asubuhi.
Agizo hilo linafuatia wasiwasi kuhusiana na aliko mwanablogu huyo baada ya kutoweka kwa muda wa zaidi ya siku kumi.
Agizo hilo la mahakama linajiri huku kukiwa na madai kutoka kwa serikali kupitia hati ya kiapo ya sajenti Samuel Itegi wa idara ya upelelezi – DCI, kwamba Kinyagia anachunguzwa kwa madai ya uchochezi wakati wa maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z.