Mwanamuziki nguli wa Uganda Bebe Cool amesimulia mengi kuhusu ndoa yake na Zuena Kirema wakati wa maonyesho ya bibi na bwana harusi nchini humo.
Akizungumza katika mahojiano kwenye siku ya mwisho ya maonyesho hayo, Bebe Cool alikanusha madai ya awali kwamba mkewe Zuena aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki aliyefariki Mowzey Radio.
Cool alielezea pia kuhusu jinsi alijipata matatani huku akichuiwa na wengi kwa sababu tu ya kujinyakulia mrembo Zuena ambaye wengi walikuwa wanamezea mate.
“Nimechukiwa na kutukanwa kwa sababu ya mke wangu Zuena, kuna watu wengi ambao walitaka kumchumbia. Walilipa hata wanablogu wanitukane,” alisema Bebe Cool.
Msanii huyo alisema kwamba alijitia tu moyo kwa sababu akipenda amependa.
Bebe Cool alitumia fursa hiyo ya mahojiano kuelezea pia kuhusu uhasama wa muda mrefu kati yake na msanii mwenza ambaye pia ni mwanasiasa Bobi Wine.
Kulingana naye, familia zao zilikuwa na uhusiano wa karibu kiasi kwamba wakati Bobi Wine alikuwa anakorofishana na mke wake Barbie, Barbie alikuwa anakimbilia kwa Bebe Cool anatulizwa na Zuena.
Wakati Bebe na Zuena walikorfishana mwaka 2009, Bebe alimpigia simu Barbie akamfahamisha huku akimwomba azungumze na rafiki yake ili waweze kurudiana.
Bobi alipofahamu kuhusu mawasiliano hayo, alimpigia simu Bebe Cool na kumzomea vikali kwa kuwasiliana na mke wake. Hata hivyo Bebe anasisitiza kwamba ugomvi ulioko ni kati yake na Bobi Wine pekee na wala sio watu wa familia yake.